BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu. Kwa furaha kubwa nakukaribisha tujifunze faida
za maombi ya kufunga. Marko 9:23 ‘’ YESU akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana
kwake aaminiye.‘’ -Kwanini Mengine yanashindwa kuwezekana? Ni kwa sababu
hatufungi na hata tukifunga basi tunafunga bila kuomba na hata tukiomba
tunaomba kidogo sana. Baada ya mimi kuokoka nilikaa siku kadhaa bila hata
kuwaza kama huwa kuna kufunga. Lakini siku moja kwa neema ya ajabu nikasikia
sauti ikisema ‘’ Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika
kinywa cha MUNGU.’’ Na baada tu kusikia sauti hiyo nikapata msukumo wa ajabu wa
kufunga. Niliazimia kufunga siku 3 hata hivyo sikuzimaliza. Lakini baadae
nilizoea na wakati mwingine nilikuwa naweza kufunga siku 3 bila kula chochote
na kazi mbalimbali nafanya lakini hawezi kujua mtu yeyote. Maombi ya kufunga ni
muhimu sana kwa kila Mkristo. Kuna watumishi hufunga siku hata zaidi ya 7 bila
kula chochote wakiomba kwa BWANA. 2 Petro 1:10 ‘’ Kwa hiyo ndugu, jitahidini
zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo
hamtajikwaa kamwe. ‘’ Kunahitajika juhudi na nguvu ili tusijikwae. juhudi hizo
na nguvu hizo wakati mwingine zinahitaji kufunga na kuomba. Luka 2:37 ‘’ Naye
ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku
na mchana kwa kufunga na kuomba. ‘’ -Maombi ni maisha kwa mkristo. -Maombi ni
mkono mrefu wa kupokea kutoka kwa MUNGU. -Kwa sababu maombi ni maisha tambua
jambo hili kwamba maombi ya kufunga ni sehemu ya maombi ambayo maombi hayo ni
maisha. -Mama huyu kweli andiko hapo juu alikuwa na miaka 84 lakini alikuwa
akifunga na kumwomba MUNGU. Kumbe kufunga ni muhimu sana kwako, kama watu wa
miaka 84 wanafunga unadhani kuna udhuru utatoa wewe mwenye miaka chini ya 40.
Kila mtu anatakiwa kuomba na wakati mwingi kuomba maombi ya kufunga. FAIDA SABA
ZA MAOMBI YA KUFUNGA. 1. Maombi ya kufunga yanaweza kukufanya uongezeke kiimani.
Mathayo 17:21 ‘’ [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.] ‘’ -Kwa
sababu kuna mambo ambayo yatawezekana tu baada ya kufunga, naamini imani yako
itaongezeka kupitia matokeo ya kufunga kwako. Mfano. Ulikuwa ukihitaji kupata
kazi kwa muda mrefu sana. Uliomba maombi ya kawaida na bado hukufanikiwa kupata
kazi, baada ya kuamua kufunga siku 5 ukajikuta unapata kazi na pia ukawa
unapigiwa simu kwamba unahitajika katika kazi 3 tofauti. MUNGU amekujibu ombi
lako la kupata kazi na nahakika imani yako itaongezeka sana. Ndio maana nasema
hivi maombi ya kufunga yanaweza kusababisha imani yako ikue, hiyo ndio sifa ya
kufunga na kuomba kisha kupokee kutoka kwa BWANA. 2. Macho yako ya ndani
yatakuwa yanaona vizuri. Zaburi 119:18 ‘’ Unifumbue macho yangu niyatazame
Maajabu yatokayo katika sheria yako. ‘’ -Mambo mengine ya kiroho kuyajua ni
lazima ufumbuliwe macho ndipo utaona na kujua. -Kuna vitu vingi sana ambavyo
sikuwahi kuvijua wala kuviona lakini baada ya maombi ya kufunga niliona na
kushangaa sana. -Biblia inaposema kwamba ''Unifumbue macho yangu nitazame''
maana yake mwanzo hakuweza kutazama na kuelewa hata kama macho anayo ila macho
ya ndani yalikuwa yamezibwa ndio maana hakuona, na katika hilo tunarudi pale
pale kwamba ''Mengine yatawezekana tu baada ya kufunga na kuomba'' -Maombi ya
kufunga yatafungua macho yako ya ndani na na utaona hata maadui walio sirini
ambao wamekutesa kwa muda mrefu. . 3. Mwili wako utakuwa umetiishwa. Wakolosai
3:5 ‘’ Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu,
tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu;‘’ -Ndugu yangu,
kuutiisha mwili wakati mwingine hauhitaji tu kujaribu kuishi maisha matakatifu
bali ni kuishi maisha matakatifu huku ukiomba na maombi ya kufunga ndio yaliyo
na nguvu zaidi za kukusaidia katika hilo. -Unapofunga na kuomba hata kama
hukuombea kutiisha mwili wako lakini lazima tu mwili wako utiishwe kutokana na
maombi uliyoomba hata kama hukuombea jambo hilo. -Maombi ya kufunga ni tiba kuu
ya vitu vinavokutesa ambavyo viko katika mwili wako. -Kama unateswa na mwili
wako kwa kuwaka tamaa ya ngono, basi funga na kuomba na mwili wako uttiishwa.
-Kama mawazo mabaya yanakutesa basi funga na kuomba yataondoka. -Kitu chochote
ambacho kinakuendesha bila hata wewe binafsi kutaka, lakini unajikuta tu
ukikitii kitu hicho ambacho ni machukizo, basi funga na kuomba utashinda. 1
Thesalonike 5:17 ''ombeni bila kukoma;'' -Njia mojawapo ya kuutiisha mwili wako
hata usinaswe na dhambi wala tamaa mbaya ni kwa njia ya kufunga. -Kama umekuwa
unateswa na mawazo machafu yanayokunajisi basi ukifunga na ukaomba kweli katika
kufunga kwako hakika mawazo hayo machafu yataondoka. -Kufunga ni muhimu sana
kwa wewe ambaye dhambi za zamani zinataka kukuteka tena. Funga na omba hakika
utabaki mshindi daima. Marko 11:24 ''Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote
myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.'' 4.
Kupokea maana ni ahadi ya MUNGU kujibu maombi yako. Yeremia 29:13 ‘’Nanyi
mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.'' Tena Biblia
inasema ''Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi
mtafunguliwa;-Mathayo 7:7'' na kwa sababu MUNGU analiangalia neno lake
alitimize basi hata aliposema tuombe ni hakika atajibu maana yeye hajipingi na
Neno lake, labda tu sisi tuombe vibaya na tupungukiwe na imani katika maombi
yetu. 1 Yohana 5:14-15 ''Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba
kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia,
tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.'' -Maombi ya
kufunga ni mkono mrefu wa kupokea kutoka kwa MUNGU. Waebrania 4:16 ''Basi na
tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya
kutusaidia wakati wa mahitaji. '' 5. Utamruhusu ROHO MTAKATIFU kukutumia. 1 Kor
12:11 ‘’ lakini kazi hizi zote huzitenda ROHO huyo mmoja, yeye yule, akimgawia
kila mtu peke yake kama apendavyo yeye. ‘’ -ROHO MTAKATIFU humgawia kila mtu
huduma kama atakavyo yeye ROHO lakini wakati mwingine huduma unayo lakini
haiendelei kwa sababu huombi ndio maana BWANA YESU akasema '' Mengine
yatawezekana kwa wewe kufunga na kuomba'' -Maombi ya kufunga ni muhimu sana na
inakuwa rahisi zaidi ROHO MTAKATIFU kukutumia maana hata wewe unakuwa rohoni.
-ROHO pia anaweza kukutumia kwa maombi. Warumi 8:26-27 ''Kadhalika ROHO naye
hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini ROHO
mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo
aijua nia ya ROHO ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo MUNGU''.
6. Utatumika kwa MUNGU vizuri Matendo 13:2-3 ‘’Basi hawa walipokuwa wakimfanyia
BWANA ibada na kufunga, ROHO MTAKATIFU akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa
kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu
yao, wakawaacha waende zao.’’ -Maombi ya kufunga yalifungulia njia ya watumishi
hawa kuitwa na kupewa jukumu na MUNGU. -Hata wewe unaweza kuwa katika kufunga
na MUNGU akasema na wewe jambo fulani ambalo unatakiwa ulitende, unaweza
kujiuliza kwanini ROHO hakusema wakati hawakufunga na kuomba? Maombi ya kufunga
ni muhimu sana. 7. Utakuwa na nguvu za MUNGU. Mathayo 11:12 ‘’Tangu siku za
Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye
nguvu wauteka.‘’ -Ndugu, watu wenye nguvu tu ndio wanaouteka ufalme wa MUNGU.
nguvu zinazozungumzwa hapa sio nguvu za miili ila ni nguvu za rohoni ambazo
hupatikana kwa kujifunza neno la kulijua, kuishi maisha matakatifu, kumtumikia
BWANA YESU na kuomba sana. na maombi ya kufunga ndio maombi ambayo yatakufanya
uwe na nguvu zaidi za rohoni hata shetani asikurudishe nyuma. ''Kama
ningaliwaza maovu moyoni mwangu, BWANA asingesikia. Hakika MUNGU amesikia;
Ameisikiliza sauti ya maombi yangu-Zaburi 66:18-19'' -Ndugu,Naamini umejifunza
na utachukua hatua njema ya kumpokea BWANA YESU kama hujaokoka ili awe BWANA na
MWOKOZI wako tangu leo na utaanza kuishi maisha matakatifu KAMA UNATAKA KUTUBU
RUDIA MANENO HAYA KISHA TAFUTA KANISA LA KIROHO UKAJIUNGE NA KUANZA KUISHI
MAISHA MATAKATIFU. ''BABA katika jina la YESU KRISTO Niko mbele zako mimi
mwenye dhambi, lakini leo nimetambua kosa langu na naomba unisamehe dhambi
zangu zote, nisamehe dhambi ninazozikumbuka na pia zile ambazo sizikumbuki.
futa jina langu katika kitabu cha hukumu na uliandike jina langu katika kitabu
cha uzima. Neno lako katika Warumi sura ya 10 Mstari wa 9 na wa 10 Neno lako
linasema ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na
kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana
kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu
'' . BWANA YESU mimi nimekuamini leo na hivyo naamini sasa napokea wokovu wako
na hakika nimeokoka. Kuanzia leo Naufunga ukurasa wa dhambi na ninaufungua
ukurasa wa matendo mema na matakatifu. BWANA nipe ROHO wako Mtakatifu ili
aniwezeshe kushinda dhambi na anasa zote za dunia. Kuanzia leo mimi nimeokoka
na ni mtoto wa MUNGU mwenye haki zote. ninafuta laana zote na kila roho ya
shetani inayonifuatilia naiharibu kwa jina la YESU KRISTO kama neno la MUNGU
linavyosema katika Yeremia sura ya kwanza mstari wa 10. BWANA YESU nakushukuru
sana kwa kuniokoa. Yote haya kwa imani nimepokea na niko tayari sasa kwa ROHO
MTAKATIFU kunitumia. Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea Amen.''
Kama umetubu toba ya kweli hakika wewe kuanzia sasa ni mshindi na ni shujaa.
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.
ulishindwa kumpokea BWANA YESU nafasi yako bado ipo na muda wa kumpokea ni leo
wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na
utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na
wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU
akubariki sana . Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula +255714252292 mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
No comments:
Post a Comment