NITAISHINDAJE DHAMBI INAYONITESA? Na
Mtumishi Peter Mabula. Ni ujumbe alioniandikia ndugu mmoja ambaye alihitaji
msaada wa kiroho. Ndugu huyu alianiandikia hivi; Hallo Peter Mabula mtumishi wa
MUNGU. kwanza namshukuru MUNGU kwa kuyapitia mafundisho yako, kwani kwa muda
mrefu nimekuwa nikifikiria njia ya kuacha uzinzi kwani sioni FAIDA yake lakini
kila nikijitahidi kuacha najikuta nimetumbukia tena na moyo unaniuma sana kwani
nilikuwa NIMEOKOKA na kwa kweli nilikuwa na matamanio mkubwa ya kumtumikia
Mungu na sasa hayapo kabisa na kwa kweli uvivu katika kumtafuta Mungu mara kwa
mara umenifanya nirudi nyuma na kila nkijitahidi kusimama najikuta narudi nyuma
kweli inaniumiza Imefika mahali nimekata tamaa kabisa hata ya kwenda kanisani
na hata nikitamani kwenda kanisani nakuta moyo unanirudisha ; Na isitoshe kila
nikifikiria maovu niliyomtenda Mungu naona kabisa kama sina nafasi kwake, kwa
mtu niliyemjua na kuanza kutenda maovu mabaya ingawa natamani sana nirudi kwake
Na mbaya zaidi kweli wakati mwingine nimekuwa nikiomba maombi kwa watumishi wa
MUNGU kuomba sala ya toba lakini najikuta narudi tena kulekule hivyo naona kama
namtania Mungu na kuingia kanisani nkiwa mwenye dhambi naona kama kumfanyia
masihara muumba naomba ushuri wako. Baada ya mimi Peter Kuusoma ujumbe wa ndugu
huyo hapo juu nilimjibu na kuahidi kuanza kumuombea. Majibu yangu hayo nataka
yakusaidie na wewe ili umpokee BWANA YESU na kusimama imara katika wokovu wa
BWANA. Majibu yangu ni haya; ubarikiwe kwa kunieleza siri yako inayokutesa kwa
muda mrefu. Naomba nikushauri kama ifuatavyo; Kuacha dhambi kwa mtu yeyote huja
baada ya mtu huyo kuamua kuipenda mbingu badala ya jehanamu. Ukijua kwamba kuna
ziwa la moto ambalo waovu wataenda huko milele basi utakuwa na sababu kuu ya
kuamua kubadilika. ''Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu
cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.-Ufunuo 20:15'' Biblia iko wazi
kabisa juu wa watenda dhambi wasio tubu kwamba kuna ziwa la moto. Nakuomba kama
hilo kanisa ambalo uliokokea mwanzo liko karibu basi muone mchungaji na mweleze
kisha atakuongoza sala ya toba na utaanza upya na BWANA YESU. ''Ungameni dhambi
zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki
kwafaa sana, akiomba kwa bidii.-Yakobo 5:16 '' Kama uko mkoa mwingine au uko
mbali na huko basi tafuta kanisa la kiroho kisha amua tu kuokoka kwa upya.
Kulikwepa kanisa hakuwezi kukusaidia kitu chochote. Kumuonea aibu MUNGU kwa
kulikimbia kanisa lake ni kuonea aibu uzima wa milele. ''Kwa sababu, ukimkiri
YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU
alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata
haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila
amwaminiye hatatahayarika.-Warumi 10:9-11'' Binafsi nitakuombea juu ya MUNGU
kukusaidia katika hilo jambo lakini pia maamuzi ya jinsi ya kuishi yako kwako
mwenyewe. Wengi husema vishawishi ndivyo vilivyowapelekea kufanya dhambi,
wengine husema ujana na wengine husema shetani lakini mimi nakuambia kwamba
mhusika mwenyewe ndio huwa chanzo cha uovu wake. Yohana 3:18-21 '' Amwaminiye
yeye(YESU) hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini
jina la Mwana pekee wa MUNGU. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja
ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa
maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru,
matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili
matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika MUNGU.'' Kama ukiambiwa
chakula kilicho mbele yako kina sumu hakika hutakula hata kama ni kwa
kulazimishwa hutakubali. dhambi ni mbaya kuliko sumu maana dhambi inaweza kuzaa
jehanamu hivyo kama tunaiogopa sumu kwenye chakula basi tuogope na dhambi kwa
namna hiyo hiyo maana dhambi ina madhara makubwa sana zaidi ya sumu. Nakuomba
okoka kwa upya kisha fanya yafuatayo; 1. Jitenge na marafiki wabaya
waliokusaidia mwanzo wewe kuingia dhambini. 2. Hakikisha unakuwa mhudhuliaji wa
kila kipindi cha ibada kanisani kuanzia katikati ya wiki na jumapili pia. 3.
Tendea kazi Neno la MUNGU unalofundishwa kanisani. 4. Uwe muwazi kwa baba yako
wa kiroho ili akusaidie kwa ushauri na maombi. 5. Jiunge na kundi la maombi
kanisani na hakikisha unakuwa muombaji maana kazi mojawapo ya maombi ni
kututiisha mwili ili tamaa zisikusumbue. 6. Amua kuwa kiumbe kipya kisicho
husika na dhambi maana ukiwa na nia hiyo ROHO MTAKATIFU atakuja kwako na
kukusaidia jinsi ya kuishi ili ubaki katika utakatifu. 7. Jiunge na huduma
kanisani ili jambo hilo likusaidie kuwa busy na huduma na kwa kuwa kwenye
huduma kutakusaidia wewe kuwa kwenye mtandao mkubwa wa kuombewa mara kwa mara
na wana kanisa. Mfano ukijiunga na kwaya itakuwa kwako rahisi kuombewa maana
wanaoombea huduma za kanisani ni wengi. 8. Sahau mambo ya nyuma na yafute
kabisa kwenye akili yako ili yasikufanye ukose ujasiri wa kuendelea mbele. 9.
Hakikisha unakuwa kielelezo cha matendo mema. 10. Liishi Neno la MUNGU siku
zote. Mathayo 13:41-43 '' Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao
watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na
kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo
wenye haki watakapong'aa kama jua katika ufalme wa BABA yao. Mwenye masikio, na
asikie. '' Ndio maana Biblia siku zote inatushauri kwamba ''Tubuni basi,
mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako
kwake Bwana;-Matendo 3:19'' Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo
la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba
tubu na okoka. Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo
kuishi maisha matakatifu ya wokovu. Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha
yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi
sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa
milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu. MUNGU wangu akubariki
sana na akupe ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe ufahamu wa kuliishi
kusudi lake jema kwako. ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo yangu. Ni mimi
ndugu yako Peter M Mabula. 0714252292. mabula1986@gmail.com Ubarikiwe sana kwa
kusoma somo hili.
No comments:
Post a Comment